Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema majeraha imekuwa changamoto kubwa ya kikosi chake kuelekea mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumamosi
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo mapema leo, Gamondi alisema hana uhakika wa kupata huduma ya wachezaji watatu hadi wanne jambo ambalo ni pigo kwa kikosi chake
"Wachezaji kama Khalid Aucho, Yao Kouassi na Pacome Zouzoua ni majeruhi pamoja na Kibwana Shomari ambaye licha ya kuanza mazoezi bado hayuko fit"
"Pia bado sijawaona Aziz Ki na Diarra ambao niliarifiwa wanarudi leo asubuhi kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa, hali hii inatupa ugumu katika maandalizi ya mchezo wetu na Mamelodi kulingana na hali ya kikosi," alisema Gamondi
Pamoja na changamoto hizo Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na ni suala la wachezaji wake kuwa sawa kisaikolojia na kuipambania nembo ya klabu ya Yanga
"Licha ya kukosa nyota wangu kwenye maandalizi, nina imani na Wachezaji wengine ambao wapo kambini. Jambo muhimu ni kujitoa zaidi, kuliko Mamelodi. Sisemi kuwa hatuwafikii uwezo Mamelodi, ila naamini wana Wachezaji wenye uzoefu mkubwa hivyo ni lazima vijana wangu wajitoe zaidi"