Yanga imempa Mudathir Yahya jukumu la kubeba hamasa kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya mamelodi Sundowns ambao utapigwa Jumamosi, March 30 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Wakati akimtangaza jana, msemaji wa Yanga Ali Kamwe alibainisha kuwa jina la Mudathir halikuzuka tu, limepitishwa na wachezaji wenzake na hata benchi la ufundi wakiamini ndiye mtu sahihi kubeba mechi kubwa dhidi ya Mamelodi
Ndani ya uwanja, Mudathir ni mmoja wa wachezaji bora kabisa wa kikosi cha Yanga msimu huu
Pengine huu ndio msimu wake bora kuliko wakati mwingine wowote katika maisha yake ya kutandaza kabumbu
Akitumika kama kiungo huru anayekwenda mbele na kurudi (box 2 box), Mudathir amepachika mabao 10 na kutoa pasi mbili za mabao
Ana mabao nane kwenye ligi kuu na mabao mawili katika ligi ya mabingwa (CAF CL)
Msimu huu Mudathir aliibeba Yanga katika baadhi ya mechi akifunga mabao muhimu yaliyoipatia Yanga alama tatu au kuongeza ari ya kikosi
Kuna alama 9 Yanga ilikusanya kwenye ligi kutokana na mabao yake ya dakika za lala salama lakini pia alifunga bao la kwanza la Yanga katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya CR Belouizdad
Ni bao hilo ambalo liliifungua CR Belouizdad na kujikuta ikiruhusu mabao mengine matatu yaliyoipa tiketi Yanga kutinga robo fainali ya ligi ya mabingwa baada ya ushindi wa mabao 4-0
Mudathir ni mchezaji anayemwagika jasho jingi katika eneo la kiungo, aina yake ya uchezaji inaweza kuwa chachu ya kuwafanya wachezaji wengine wajitume zaidi katika mchezo dhidi ya Mamelodi
Pamoja na sifa nyingi wanazopewa wachezaji wa Mamelodi hasa katika eneo la kiungo lakini kama watakutana na Mudathir akiwa katika ubora wake, akishirikiana na kina Maxi Nzengeli, Khalid Aucho, Pacome na wengine watakaokuwa katika eneo la kiungo, kwa hakika hawataisahau March 30