Meneja wa Yanga Walter Harrison amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa timu hiyo juu ya hali za wachezaji Pacome Zouzoua na Yao Kouassi ambao jana walipata majeraha katika mchezo wa ligi kuu ya NBC dhidi ya Azam Fc ambao Wananchi walikubali kipigo cha mabao 2-1 uwanja wa Benjamin Mkapa
Walter amesema uchunguzi wa awali unaonyesha wachezaji hao walipata majeraha ya kawaida hivyo anaamini watakuwa tayari kuikabili Mamelodi Sundowns March 30 katika mchezo wa ligi ya mabingwa
"Niwatoe hofu juu ya wachezaji wetu Pacome na Yao, walipata majeraha lakini hali zao zinaendelea vizuri. Wapo katika uangalizi wa madaktari wetu na naamini mpaka kufikia siku ya mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns, watakuwa tayari kuwapa furaha Wananchi," alisema Walter
Akizungumzia mchezo dhidi ya Azam Fc, Walter aliseema wamekubali matokeo ya kupoteza mchezo huo ingawa malengo yao ilikuwa kushinda
"Nawapongeza Azam Fc kwa kuibuka na ushindi leo, ndivyo mpira wa miguu ulivyo zipo nyakati za furaha na huzuni"
"Tumekuwa na ratiba ngumu kidogo, tumecheza mechi nne katika siku 12, tumevuna alama 9 kati ya 12 sio jambo dogo. Ligi ni marathon bado tunayo nafasi ya kutetea ubingwa wetu, tutahakikisha tunafanya vizuri katika mechi 10 zilizosalia"