Tumeisikia kauli ya Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars Hemedi Morocco akisema kuwa beki Dickson Job hana nafasi katika kikosi chake kwa kuwa sio aina ya mabeki ambao anawahitaji kutokana na kimo chake
Morocco aliyazungumza hayo baada ya wadau mbalimbali wa soka kuhoji sababu ya kumuacha Job katika kikosi cha Stars licha ya beki huyo kuwa katika kiwango bora
Ukichunguza kwa makini, kauli hiyo ndio sababu ya Job kutojumuishwa na sio tuhuma za utovu wa nidhamu kama alivyozungumza awali. Utovu wa nidhamu ni kichaka tu cha kujificha
Kauli ya Morocco inashangaza kwa sababu Job amekuwa sehemu ya kikosi cha Stars tangu mwaka 2015. Job amefundishwa na makocha wenye profile kubwa kuliko Morocco lakini hawakuwahi kutoa kauli kama yake
Katika klabu ya Yanga Job ni panga pangua katika kikosi cha kwanza, amecheza mechi kubwa na zenye ushindani, tatizo la kimo halikuwahi kuonekana
Kocha ni kama mzazi, kutoka hadharani na kutamka kuwa simtaki mchezaji fulani kwenye timu yangu kwa kuwa ni mfupi, sio uungwana na ni kumkosea mchezaji ambaye ameitumikia timu ya Taifa tangu akiwa kinda
Kauli ya Morocco inatupa taswira ya aina ya unyanyapaa ambao pengine Job amekutana nao katika kikosi cha Stars na utaelewa kwa nini hakuwa tayari kucheza nafasi ambayo alipangwa na kocha huyo wakati wa Afcon 2023
Wananchi tunajua Job ni beki wa daraja la juu na hakuwahi kuwa tuhuma zozote za utovu wa nidhamu tangu ajiunge na Yanga