Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wamejipanga kuendeleza kasi yao ya kuzifumania nyavu katika ligi kuu ya NBC pale watakapoikabili Geita Gold uwanja wa Azam Complex hapo kesho
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Gamondi amesema anafahamu mbinu ambayo Geita Gold watakuja nayo, lakini hawahofii kwa sababu ana kikosi bora
"Mechi tatu tumefunga magoli 15, tumeruhusu bao 3, kimsingi hizi ni takwimu bora"
"Siwezi kusema kwamba Geita nao tutawafunga magoli mengi huo utakuwa ubashiri sifanyi kazi ya kubashiri, ninachoweza kufanya kwa sasa ni kujiandaa kushinda mchezo"
"Tumejiandaa kucheza nao kwa namna yoyote ambayo watajipanga, nafikiri watakuja na mbinu za kujilinda lakini hainipi hofu kwa sababu nina vijana wazuri," alisema Gamondi
"Tunafahamu kila mpinzani kuna namna yake ya kujiandaa kimbinu, Ukitazama matokeo yao ya hivi karibuni wameimarika hivyo lazima tuchukue tahadhari ya kutosha bila kujali matokeo yetu ya awali"
"Nina wachezaji wengi wazuri sana, tunaweza kucheza aina yoyote ya mchezo, iwe kushambulia, kumiliki mpira nk. Tunaweza kubadilika badilika kulingana na matakwa ya mchezo kabla na wakati wa mchezo, sijawahi kucheza na aina moja ya falsafa huwa nabadilika kulingana na namna mpinzani anavyocheza na namna navyoweza kummudu, " aliongeza Gamondi