Wananchi wanahesabu saa kabla ya kuelekea dimba la Kimataifa ya Cairo kumenyana na Al Ahly katika mchezo wa kuhitimisha kundi D michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Ni mechi ya aina yake kwa sababu inakutanisha timu ambazo mkononi tayari zina tiketi ya kucheza robo fainali. Hivyo utakuwa mchezo wa kusimika timu itakayoongoza kundi
Ili kumaliza katika nafasi ya kwanza, Yanga ni lazima ishinde mchezo huo. Hivyo ni mchezo ambao Yanga itakuwa ikisaka ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Al Ahly
Mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa ilimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, Pacome Zouzoua akiisawazishia Yanga katika dakika za lala salama
Licha ya kucheza kwa ushindani katika mechi za nyuma ambazo Yanga imewahi kucheza dhidi ya Al Ahly nchini Misri, Wananchi bado hawajaandikisha ushindi ugenini dhidi ya wababe hao wa soka barani Afrika
Hivyo kama Yanga itafanikiwa kushinda leo basi itakuwa rekodi mpya kwa Wananchi
Rekodi ambayo itatuma salamu kwa timu nyingine zinazoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu kuwa zisitamani kukutana na Wananchi
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesisitiza kuwa hawana hofu yoyote kuelekea mchezo huo
Amesema wanakwenda kuwaonyesha Al Ahly kile walichokiandaa kutoka katika uwanja wa mazoezi