Winga wa Yanga,raia wa Ghana Augustine Okrah amesema baada ya kupona majeraha aliyoyapata kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi 2024 sasa amerejea kwenye utimamu wake na kadri siku zinavyoenda anazidi kuimarika
Okrah alitua Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu na tayari ameanza kuonyesha makeke yake kikosini hapo akitoa asisti mbili kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ambao Yanga ilishinda 5-0 dhidi ya Polisi Tanzania
Katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya CR Belouizdad dakika chache alizocheza katika kipindi cha pili ziliwasisimua Wananchi waliotamani kila wakati apewe mpira kwa jinsi alivyokuwa akipepea katika wingi ya kulia
Okrah amesema baada ya afya yake kuimarika, anaamini atapata muda wa kutosha kuwatumikia Wananchi
"Awali nilikuwa na majeraha, hivyo sikupata muda wa kucheza. Ukitoka kwenye majeraha hauwezi kuingia moja kwa moja kikosini, namshukuru Mungu napata nafasi na kucheza na naamini kadri siku zinavyozidi kwenda naimarika zaidi na nitapata muda zaidi wa kucheza na kuonyesha ubora wangu,” alisema Okrah
Kabla ya kutua Yanga, Okrah alikuwa akicheza klabu ya Bechem United ya kwao Ghana ambapo katika mechi 16 alizocheza alicheka na nyavu mara tisa
Yuko sehemu ya kikosi kinachoendelea na maandalizi ya kuikabili Al Ahly nchini Misri hapo kesho
Okrah ana nafasi kubwa ya kuanza mchezo huo kutokana na majeraha ya kiganja aliyopata Maxi Nzengeli katika mchezo dhidi ya Belouizdad
Nzengeli pia yuko sehemu ya kikosi lakini huenda Mkufunzi wa Yanga Miguel Gamondi asimtumie katika mchezo dhidi ya Al Ahly au kumpa dakika chache