Klabu ya Yanga leo Jumatatu, Februari 05 imeingia katika maadhimisho ya wiki ya Yanga ambayo kilele chake ni Februari 11
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema Februari 11 Yanga inatimiza miaka 89
Mwaka huu uongozi wa Yanga umeamua kuadhimisha siku hiyo kwa utaratibu tofauti. Yanga imeandaa matukio mbalimbali katika wiki hii ikiwa ni pamoja na kusaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano na Taasisi mbalimbali
"Leo rasmi tumeingia kwenye wiki ya anniversary ya Klabu hii kubwa Tanzania kuelekea kilele cha Birthday ya Young Africans SC tarehe 11 mwezi huu wa pili, safari hii tuna mambo makubwa. Hii ni wiki yetu wenyewe"
"Kesho Young Africans SC tutakwenda kusaini mkataba na Hospitali kubwa sana duniani, ikiwa na lengo la kumnufaisha shabiki wetu kwenye masuala yanayohusu afya yao. Klabu kubwa lazima iwaze kwa ukubwa namna gani Mwanachama wake atanufaika na Klabu kubwa," alisema Kamwe
Tukio jingine kubwa litakalofanyika katika wiki ya Yanga ni uzinduzi wa Makao Makuu ya klabu ya Yanga baada ya kufanyika ukarabati mkubwa. Tukio hilo litafanyika siku ya Jumatano
Kamwe amesema katika uzinduzi huo Wananchi watashuhudia Makao Makuu bora zaidi ya klabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
"Siku ya jumatano, pale makao makuu ya Jangwani, tunakwenda kuzindua upya ofisi zetu. Uongozi wa klabu yetu umefanya ukarabati wa kihistoria. Ukarabati huo umeifanya Klabu ya Young Africans SC kuwa na ofisi bora zaidi AFRIKA MASHARIKI NA KATI"
Kilele cha maadhimisho ya miaka 89 ya Yanga itafanyika mkoani Mbeya ambapo Yanga itachuana na Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa uwanja wa Sokoine
Kamwe amewataka Wanachama na Mashabiki wa Yanga kuanza safari kuelekea mkoani Mbeya ili kuhakikisha maadhimisho ya miaka 89 ya klabu yanafana