Mshambuliaji wa Yanga Hafiz Konkoni amewaaga wachezaji wenzake akiwa mbioni kuondoka nchini kuelekea klabu ya Dogan Turk Birligi ya Cyprus kwa mkopo mpaka mwisho wa msimu
Konkoni amebainisha kuwa alitamani kuendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga lakini haikuwezekana na hivyo kulazimika kuondoka ili kupaa nafasi ya kucheza sehemu nyingine
Mshambuliaji huyo ameongeza kuwa, anaondoka Yanga akiwa bado anaipenda na anaumizwa na deni la kushindwa kutimiza malengo ya usajili wake
"Haikuwa muda sahihi kwangu kuondoka Yanga, bado nina deni kubwa kwa mashabiki kwa vile sikupata nafasi ya kuitumikia vya kutosha, lakini sina namna. Nimewaaga wachezaji wenzangu pamoja na kocha na kuitakia kila la kheri timu mimi nakwenda kuanza maisha mapya katika timu nitakayoitumikia," alisema
Hadi anaondoka Yanga, Konkoni alifunga mabao mawili tu, likiwamo moja la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC na jingine kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti iliyofumuliwa mabao 5-1
Nafasi yake imezibwa na mshambuliaji mpya Joseph Guede kutoka Ivory Coast aliyetambulishwa muda mchache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Jumatatu usiku, akiwa ni mchezaji wa pili baada ya Mghana Augustine Okrah aliyechukua nafasi ya Jesus Moloko aliyeachwa
Yanga pia ilimsajili nyota wa ndani kinda Shekhan Khamis kutoka klabu ya JKU huku pia ikimtoa kwa mkopo Crispine Ngushi kwenda klabu ya Coastal Union