Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto jana alikuwa katika kiwango bora akiiongoza Yanga kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama Fc katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika
Ulikuwa mchezo ambao Yanga ilihitaji ushindi na kwa hakika Mwamnyeto aliwaongoza vyema wenzake uwanjani kupambana na kuhakikisha ushindi huo unapatikana
Wapo wanaweza kuzungumzia uhusika wake katika penati waliyopata Medeama lakini ni sehemu ya mchezo
Jana Mwamnyeto alifanikiwa zaidi kumdhibiti mshambuliaji tegemeo wa Medeama Jonathan Sowah kuliko kosa hilo moja alilofanya
Kama ni alama, basi Mwamnyeto alipata alama nyingi zaidi katika safu ya ulinzi, umahiri wake katika kuanzisha mashambulizi ilikuwa kitu kingine cha kipekee
Lakini pia akahusika katika bao la pili la Yanga lililofungwa na Kennedy Musonda baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Musonda kumgonga na kumpoteza mlinda lango wa Medeama
Hata hivyo bao hilo amepewa Musonda kwa kuwa mpira wake aliopiga kwa kichw ulikuwa 'on-target' kabla ya kumgonga Mwamnyeto
Ushindi waliopata Yanga jana ulikuwa na thamani kubwa kwani umerejesha matumaini ya kufuzu robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Sasa Yanga itahitaji kushinda mchezo utakaofauata nyumbani dhidi ya CR Belouizdad matokeo ambayo yanaweza kuwapeleka Wananchi moja kwa moja robo fainali hasa ikitokea Belouizdad wakapoteza mchezo dhidi ya Al Ahly ambao uliahirishwa kutokana na Al Ahly kushiriki michuano ya FIFA Club World Cup