Oktoba 04 2023 uwanja wa Highland Estates Mbarali mkoani Mbeya Yanga ilipoteza mchezo wa ligi kuu msimu huu kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu Fc
Katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi alifanya mabadiliko ya takribani wachezaji sita katika kikosi chake kilichoanza
Baadhi ya wachezaji walioanza katika mchezo huo ni pamoja na Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Zawadi Mauya, Jesus Moloko, Salum Abubakar 'Sure boy' na Skudu
Baada ya mchezo baadhi ya mashabiki wa Yanga walimtupia lawama Gamondi kwa kufanya 'rotation' ya kikosi chake katika mchezo ambao walihitaji kushinda kutokana na kumbukumbu ya kupoteza mchezo katika uwanja huo huo msimu uliopita
Lawama kama hizo zimeanza kusikika tena baada ya Yanga kukosa ushindi katika mechi tatu za kwanza ligi ya mabingwa barani Afrika
Lakini wakati huu ni tofauti, lawama ni kwa nini kocha hafanyi 'rotation', yaani kwa nini hawatumii baadhi ya wachezaji?
Hapa ndipo kama mdau wa soka nachanganyikiwa! Ni ngumu kuelewa mashabiki wanataka nini?
Jambo hilohilo likifanyika leo watalaumu kwa nini limefanyika lakini lisipofanyika kesho watalaumu kwa nini halikufanyika?
Katika moja ya mahojiano yake wakati anakabidhiwa majukumu ya kuinoa Yanga, Gamondi aliweka wazi msimamo wake kuwa kila mchezaji ana nafasi ya kucheza katika kikosi chake muhimu ahakikishe anathibitisha utayari wake katika kiwanja cha mazoezi
Yanga ina takribani wachezaji 28, katika mechi wanaweza kucheza wachezaji 16 tu (11 wanaanza na sub ni 5)
Lakini pia kila kocha ana mfumo wake ambao anapenda timu yake icheze hivyo uchaguzi wa kikosi chake utazingatia aina ya wachezaji ambao wanafit katika mfumo huo
Hivyo wakati mwingine kufananisha kile alichofanya kocha Nasreddine Nabi na anachofanya Gamondi sasa sio sawa kwani ni makocha wenye mifumo tofauti
Katika misimu yake miwili na nusu Nabi aliipa Yanga mataji yote ya ndani pamoja na kucheza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Lakini Nabi hakuweza kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa kitu ambacho Gamondi ameweza
Gamondi kikosi chake kinafanya vizuri sana kwenye ligi, lawama anazoshushiwa ni kwa sababu amekosa ushindi katika ligi ya mabingwa
Michuano ya Ligi ya Mabingwa sio rahisi kama wengi wanavyofikiria, angalia mechi za mzunguuko wa tatu, ni mechi tatu tu zilizotoa mshindi mechi nyingine tano ziliisha kwa matokeo ya sare
Mabingwa watetezi Al Ahly wamecheza mechi mbili mfululizo pasipo kushinda. Walitoka droo na Yanga na CR Belouizdad.
Kabla ya kumfunga Simba; Wydad alipigwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Jwaneng Galaxy na Asec Mimosas
Ahly na Wydad ndio timu bora Afrika! Ahly yuko nafasi ya kwanza na Wydad nafasi ya pili. Mamelodi Sundowns hajashinda mechi mbili mfululizo, alipigwa na Mazembe na kutoka sare na Pyramids. Baada ya mzunguuko wa tatu kukamilika, hakuna timu iliyoshinda mechi zote
Wananchi watafanya makosa makubwa kutaka kumhukumu Gamondi kwa mechi hizi za Kimataifa katika mashindano ambayo kila timu inahaha kupata alama tatu
Kimahesabu bado Yanga ina nafasi nzuri ya kwenda robo fainali kwani ina mechi mbili nyumbani ambazo kama watachanga karata zao vyema zinaweza kuwapeleka hatua inayofuata