Licha ya sare ya bao 1-1 katika mchezo dhidi ya Medeama Fc uliopigwa Ghana jana, nafasi ya kufuzu robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa bado iko mikononi mwa Yanga
Hesabu za Wananchi sasa ni kuhakikisha alama sita zinapatikana katika mechi mbili zinazofuata nyumbani dhidi ya Medeama na CR Belouizdad
Kama Yanga itashinda mechi hizo mbili itafikisha alama nane ambazo pasipo na shaka zitawapeleka Wananchi katika nafasi mbili za juu kabla ya mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly
Jana Yanga iilikuwa na nafasi nzuri ya kushinda mchezo dhidi ya Medeama lakini kwa mara nyingine ikadhihirika kwa nini sio rahisi kushinda ugenini katika soka la Afrika
Kama kungekuwa na VAR, bao alilofunga Nickson Kibabage katika kipindi cha pili lingekuwa halali lakini pia pengine Medeama wasingemaliza wachezaji 11 uwanjani, kulikuwa na kadi nyekundu kwa mlinzi wa kulia wa timu hiyo aliyemfanyia rafu mbaya Kibabage kwenye kipindi cha kwanza
Waamuzi hawakumudu mchezo huo, maamuzi yao mengi yaliwapa faida wenyeji hata kwa mipira ya kugombea ambayo walinzi wa Yanga walikuwa wakiishinda kihalali
Kocha Miguel Gamondi alifanikiwa katika mpango wake wa mechi kwani Yanga ilicheza kwa tahadhari kubwa, hakukuwa na makosa mengi sana katika safu ya ulinzi huku Yao na Kibabage wakitumika ipasavyo kushambulia kutokea pembeni
Yanga inapaswa kujiandaa vyema kuhakikisha inashinda mechi mbili zinazofuata nyumbani kwani alama hizo sita zinaweza kutosha kuwapeleka Wananchi robo fainali