Mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Medeama leo utakuwa kama fainali hasa ikizingatiwa Yanga inazihitaji sana alama tatu kama ilivyo kwa wapinzani wao, Medeama Fc
Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Baba Yara jijini Kumasi ambao ni mji ambao una kadiriwa kuwa na watu 3.348 Milioni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2020 nchini humo.
Kocha wa Yanga Miguel Gamondi licha ya kukiri kwamba mchezo utakuwa mgumu alisema wamejipanga na watacheza kwa nidhamu na kuweka mipango ya kuwaondolea Medeama hesabu za ushindi.
Nje ya uwanja tajiri wa Yanga Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ na uongozi wa klabu hiyo umecheza mechi hiyo kwa akili wakiweka ahadi nzito. Kama Yanga itashinda kila bao la mchezo huo litanunuliwa kwa Sh100 milioni na idadi ya mwisho ya mabao hayo kutakuwa na ziada ya Sh200 milioni
Hata hivyo Yanga inafahamu kwamba malengo yao hayo hayataweza kutimia kirahisi kwani Medeama sio timu rahisi ikiwa nyumbani, rekodi zikionyesha kwenye mechi zao tatu za nyuma za ligi ya mabingwa wameshinda zote dhidi ya Remo Stars (1-0), Horoya AC (3-1) na Belouizdad (2-1).
Yanga pia itakumbuka kwamba mara ya mwisho walipokutana na Medeama nchini humo Julai 26, 2016 kwenye mchezo wa makundi wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua kama hii walikubali kichapo cha mabao 3-1
Yanga bado inaweza kurejesha ubabe wake katika mechi za ugenini leo baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya CR Belouizdad
Kabla ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Belouizdad, Yanga ilikuwa imecheza mechi saba za mashindano ya CAF pasipo kupoteza ugenini
Lakini pia mchezo huo unachezwa katika uwanja ambao hata Medeama sio uwanja wao wa nyumbani. Uwanja wa nyumban wa Medeama ulikataliwa na CAF baada ya kukosa vigezo muhimu na hivyo kulazimika kucheza mechi zao za nyumbani katika uwanja wa Baba Yara ulioko Kumasi
Yanga ni miongoni mwa timu bora barani Afrika kwa sasa, leo ni siku nyingine ya kudhihirisha ubora huo