Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amesema mkakati wa timu hiyo ni kuhakikisha wanavuna alama muhimu ambazo zitawapa nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Juzi Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly katika uwanja wa Benjamin Mkapa matokeo ambayo yanaifanya Yanga ipate alama moja tu kutoka mechi mbili
Arafat amesema matokeo hayo hayapaswi kuwakatisha tamaa, watajipanga kusaka alama muhimu ambazo zitawapeleka robo fainali
"Tulijiwekea malengo ya kushinda mchezo dhidi ya Al Ahly lakini haikuwa hivyo, tumepata alama moja"
"Vijana wetu walipambana kusaka ushindi lakini lazima tukubali tumekutana na timu imara (Ahly) ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hii"
"Niwambie wapenzi na wanachama wetu, tumeichukua hii alama moja, tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mechi zinazofuata. Tutapambana ili kuhakikisha tunakusanya alama muhimu ili tuweze kufuzu hatua inayofuata," alisema Arafat
Ijumaa ya wiki hii Yanga itakuwa ugenini Ghana kumenyana na Medeama kisha timu hizo kurudiana jijini Dar es salaam Disemba 20
Mechi hizi mbili zinazofuata zitaamua hatma ya Yanga katika mkakati wake wa kuisaka robo fainali ya pili katika michuano ya Ligi ya Mabingwa