Ni saa chache zimebaki kabla ya Wananchi kuelekea uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mtanange wa kukata na shoka ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Yanga dhidi ya Al Ahly
Ni majira ya saa 1 usiku mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka barani Afrika utapigwa
Utakuwa mchezo wa pili kwa Yanga ambayo inahitaji kushinda ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele hatua inayofuata katika michuano hiyo
Mpaka sasa ni Yanga pekee ambayo bado haijashinda kundi D, timu nyingine zimeshatumia vyema uwanja wa nyumbani kushinda
Jana Medeama waliichapa CR Belouizdad mabao 2-1 huko Ghana na hivyo kufikisha alama tatu sawa na Belouizdad na Al Ahly ambazo zilishinda mechi zao za kwanza nyumbani
Kama Yanga itashinda leo, itafikisha alama tatu na kuwa sawa na washindani wake katika kundi
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anafahamu umuhimu wa alama tatu katika mchezo wa leo hivyo ni wazi leo atatumia kikosi chake cha ushindi
Habari njema kwa Yanga ni kurejea langoni kwa Djigui Diarra ambaye alikosa mchezo uliopita kutokana na majeraha ya bega
Ni mechi ambayo Yanga itahitaji kushambulia ili kufunga mabao lakini pia tahadhari inahitajika kwani Al Ahly watatumia zaidi mashambulizi ya kushitukiza