Mlinda lango wa Yanga Djigui Diarra amesema afya yake imezidi kuimarika na pengine anaweza kuwa tayari siku ya Jumamosi kuikabili Al Ahly katika mchezo wa pili wa ligi ya mabingwa hatua ya makundi
Diarra alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Simba uliopigwa Novemba 05 na Yanga kuibuka na ushindi wa Mabao 5-1
Mlinda lango huyo raia wa Mali alikosekana katika mchezo dhidi ya CR Belouizdad ambao Yanga walipoteza nchini Algeria kwa kufungwa mabao 3-0, wapo wanaoamini kukosekana kwake kulichangia Yanga kupoteana katika mchezo huo
Diarra amesema anasumbuliwa na maumivu ya bega na ametakiwa kupata mapumziko zaidi ili kuwa kwenye hali nzuri ya kurudi uwanjani.
"Naendelea vizuri na ninafanya mazoezi na wenzangu, tatizo langu la bega halikuwa kubwa ila lilihitaji kupata mapumziko ya muda mrefu kiasi ili kujiweka katika hali nzuri ya ushindani nafikiri muda ukifika mtaniona uwanjani"
"Siwezi kuweka wazi ni lini ila nipo kwenye hali nzuri mashabiki watarajie kuniona uwanjani muda wowote nafurahia upendo wao kwangu, nimepokea meseji nyingi kutoka kwa Wanayanga na ninawahakikishia hatutawaangusha," alisema Diarra
Kuhusu mechi iliyopita, Diarra alisema ulikuwa ni mzuri na wenye ushindani, lakini bahati haikuwa upande wao wamesahau matokeo hayo wanajipanga kwa mchezo muhimu zaidi wa Jumamosi dhidi ya Al Ahly.
"Tumepoteza, hii ni sehemu ya matokeo tumeumia, ila tunajipanga kwa mchezo mwingine ambao ni muhimu zaidi dhidi ya Al Ahly nyumbani hatuwezi kurudia makosa tunahitaji pointi zote tatu ili kurudi kwenye mstari na mashabiki wajiandae kupata ile burudani waliyoizoea"