Yanga haijaanza vyema hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad katika mchezo uliopigwa uwanja wa July 05 1962 huko Algeria
Ulikuwa mchezo ambao Yanga ilitawala lakini CR Belouizdad walitumia vyema nafasi walizopata kujihakikishia alama tatu muhimu nyumbani
Haukuwa mchezo rahisi, Belouizdad walijiandaa vyema pia wakatumia faida ya kuwa nyumbani, zipo nyakati hata waamuzi waliwapa faida katika matukio ambayo hawakustahli
Utamaduni wa soka la Afrika ni kuwa lazima utumie vyema uwanja wa nyumbani, CR Belouizdad wametumia vyema uwanja wao kupata ushindi
Sasa ni zamu ya Yanga kutumia vyema uwanja wa nyumbani katika mchezo unaofuata dhidi ya Al Ahly ambao utapigwa Jumamosi ijayo katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Ni lazima kutumia vyema uwanja wa nyumbani, Belouizdad wameionyesha Yanga kuwa inapaswa kuwa makatili kwelikweli ndani ya dakika 90 unapocheza nyumbani ili kuhakikisha alama tatu zinabaki
Mwanzo huu katika ligi ya mabingwa hauna tofauti ya msimu uliopita kwenye kombe la Shirikisho. Yanga ilianza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir na baadae kushinda mechi nne zilizofuatia na sare moja matokeo yaliyowapeleka robo fainali na Wananchi kufanikiwa kucheza fainali ya michuano hiyo
Haukuwa mwanzo mzuri kwa Kocha Miguel Gamondi lakini bila shaka matokeo haya yamempa elimu ambayo ataitumia kufanya vizuri katika mechi zinazofuata