Kwanza tukio alilofanya Khalid Aucho kumpiga kiwiko Ibrahim Ajibu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union halikuwa la kiungwana, angepewa kadi nyekundu na mwamuzi hakuna ambaye angehoji maamuzi hayo
Pamoja na kuwa alichokozwa, wachezaji wanapaswa kuhimili hasira zao na kuhakikisha wanalinda usalama wa wenzao uwanjani
Baada ya Aucho kuonyeshwa kadi ya njano katika mchezo huo wengi walitarajia hakutakuwa na adhabu nyingine zaidi dhidi yake.
Kwa nini? kwa sababu adhabu ya mwamuzi (kupewa kadi ya njano) tayari imetoka lakini kama mwamuzi asingechukua hatua (kama hakuliona tukio) basi hii adhabu ya Kamati ya kumfungia Aucho mechi tatu hakuna ambaye angehoji uhalali wake
Au kama mwamuzi angempa Aucho kadi nyekundu ya moja kwa moja ni wazi angetumikia adhabu yake pasipo kuibuliwa kwa maswali mengi
Hili sio tukio la kwanza kutokea kwenye ligi yetu na TPLB wenyewe waliwahi kutoa ufafanuzi kuwa matukio ambayo mwamuzi aliyaona na kuyachukulia hatua uwanjani basi Kamati haiwezi kutoa adhabu zaidi kwani kufanya hivyo ni kutoa adhabu mara mbili
Lakini kwa yale ambayo waamuzi hawakuyaona, Kamati itatoa adhabu kwa kuzingatia aina ya makosa yaliyofanyika
Msimu uliopita kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, beki Hennock Inonga alimchezea rafu mbaya sana Salum Abubakar 'Sure Boy' mwamuzi akampa Inonga kadi ya njano
Wadau walipohoji kwa nini Inonga hakuadhibiwa na Kamati, sababu iliyotolewa ni kuwa mwamuzi tayari alishatoa adhabu uwanjani (kadi ya njano) mchezaji hawezi kuadhibiwa mara mbili
Tukio kama hilo lilitokea katika mchezo dhidi ya Coastal Union aliyekuwa kiungo wa Yanga Yannick Bangala akifanyiwa rafu mbaya na Mtenje Albano wa Coastal Union, Mtenje alipewa kadi ya njano na hakuna hatua zaidi iliyochukuliwa
Labda kama kuna mabadiliko ya kanuni hiyo kwa msimu huu, Aucho anakuwa mchezaji wa kwanza kuadhibiwa mara mbili (refa na kamati)
Lakini pia sidhani kama ni sahihi kwa Kamati kuingilia adhabu zinazotolewa na waaamuzi uwanjani, tukiruhusu hili tutaangukia pabaya
Kuna makosa mengi sana waamuzi wanafanya kwenye ligi yetu lakini wanalindwa, zaidi wanaadhibiwa kwa kushindwa kutafiri vyema sheria za soka na sio kubatilisha kile ambacho walikiamua katika mechi husika
Kama tunataka kubatilisha yale ambayo waamuzi wanafanya uwanjani basi tusiishie kwenye kadi tu, hata yale mabao yanayokataliwa kwa kisingizio cha kuotea basi tuzirudishie timu zilizopokwa haki