Yanga ndio mabingwa wa kihistoria wa soka la Tanzania

Yanga Damu By Yanga Damu
β€’
22 Jul 2017
Yanga ndio mabingwa wa kihistoria wa soka la Tanzania
Historia ya ligi ya Tanzania inaanzia mwaka 1929 ilipoanzishwa kifukara, tu kwa sababu ya mapenzi ya watu na soka wakaamua kuungana na kuanzisha michuano ya kutafuta bingwa, ingawa ni timu za Dar es Salaam pekee zilizokuwa zikishiriki wakati huo.

Kufika mwaka 1965, ilianzishwa michuano ya Klabu Bingwa Tanzania, ambayo ilikuwa inaanzia ngazi ya Wilaya, ikichezwa kwa mtindo wa mtoano, ingawa pia katika miaka miwili ya mwanzoni, timu za Dar es Salaama pekee ndizo zilizoshiriki.

Katika mfumo huo, bingwa wa kwanza ilikuwa ni klabu ya Sunderland ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ilifanikiwa kutetea ubingwa wake msimu uliofuata, kabla ya kuutema kwa Cosmopolitan ya Dar es Salaam pia mwaka 1967.

Lakini wakati wote huo, bado Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hivyo Sunderland hawakuwahi kucheza michuano ya Afrika.

Cosmo ingekuwa ya kwanza kucheza Klabu Bingwa Afrika mwaka 1968 kama isingejitoa, lakini kwa kujitoa kwao, Yanga ilifungua historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza mwaka 1968, kabla ya kuutetea mara nne mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970, 1971 na 1972.

Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na kuitwa Simba kurejesha taji lake mwaka 1973.

Simba ilishindwa kuutetea ubingwa wake msimu uliofuata mwaka 1974 baada ya kupokonywa na Yanga katika fainali ya kihistoria iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kwa kuchapwa mabao 2-1.

Mwaka 1975 Yanga iliutema ubingwa huo kwa Mseto SC ya Morogoro, iliyoweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa nchi.

Lakini Mseto ilishindwa kuteteqa taji hilo, ikapokonywa na Simba msimu uliofuata- na Wekundu wa Msimbazi walifanikiwa kutetea ubingwa huo kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.

Siri ya kutawala kwa Simba kwenye ligi hiyo kwa miaka yote hiyo ni kuyumba kwa Yanga baada ya kukumbwa na mgogoro mkubwa 1976, uliosababisha kukimbiwa na wachezaji wote nyota, hivyo kuanza upya kabisa kuunda timu.

Ni ndani ya kipindi hicho Simba iliweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 5-0 na Yanga mwaka 1968, wakati nayo ilipowatandika watani wao hao wa jadi 6-0 mwaka 1977.

Juni 1, mwaka 1968 Yanga iliigaragaza Simba 5-0, mabao yake yakitiwa kimiani na Maulid Dilunga (sasa marehemu) katika dakika za 18 kwa njia ya penalti na 43, wakati mengine yalitiwa kimiani na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 kabla ya Kitwana Manara kupachika la kuhitimisha karamu ya mabao dakika ya 86.

Julai 19, mwaka 1977 Simba nayo ililipa kisasi kwa kuibugiza Yanga mabao 6-0, wafungaji wakiwa ni Abdallah 'King' Kibadeni aliyetikisa nyavu mara tatu katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73 na Selemani Sanga wa Yanga alijifunga dakika ya 20.

Kufika mwaka 1981, tayari Yanga ilikuwa imara tena na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara ingawa msimu uliofuata iliutema kwa Pan African.

Kuanzia mwaka 1982, mfumo wa Ligi ya Tanzania ulibadilishwa na kukawa na ligi tatu, kwanza ni Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza visiwani Zanzibar na Ligi Kuu ya Muungano.

Yaani baada ya kupatikana washindi wawili wa juu wa kila ligi, Bara na Visiwani, walikutana kwenye Ligi Kuu ya Muungano, kutafuta bingwa wa Tanzania na washindi wake.

Wakati huo, bingwa wa Ligi ya Muungano alikwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili alicheza Kombe la Washindi.

Baadaye timu ziliongezwa na kuwa tatu kila upande katika Ligi ya Muungano.

Mwaka 1983, Yanga ilirejesha taji hilo kwenye himaya yake, ingawa msimu uliofuata ililitema tena kwa Simba.

Kwa ujumla muongo mzima wa 1980, taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara lilikuwa la kukoponyana, kwani Simba nayo mwaka 1985 ilipokonywa taji hilo na Yanga, ambayo nayo ililitema kwa timu mpya katika Ligi Kuu msimu wa 1986, Tukuyu Stars ya Mbeya.

Tukuyu nayo iliwarejeshea Yanga taji lao mwaka 1987, wakati mwaka 1988 Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga ilijiingiza katika orodha ya timu zilizowahi kutwaa taji hilo.

Mwaka 1989, Yanga ilifunga orodha ya mabingwa wa muongo huo kwa kutwaa tena ubingwa wa Bara.

Simba iliibuka mwaka 1990 na kutwaa ubingwa huo, ikitoka kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita.

Kupokonyana taji kuliendelea hata kwenye muongo wa 1990, kwani Simba iliutema ubingwa huo kwa Yanga mwaka 1991.

Yanga iliutetea ubingwa huo mara mbili mfululizo katika miaka ya 1992 na 1993, kabla ya kupokonywa na Simba mwaka 1994. Simba ilifanikiwa kuutetea mara moja 1995.

Mwaka 1996 ndipo Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilipozaliwa rasmi chini ya udhamini wa Bia ya Safari Lager, bia inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ikijulikana kama Safari Lager Premier League.

Yanga ndiyo iliyokuwa bingwa wake wa kwanza. Yanga iliutetea ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo 1997 na 1998.

Mwaka 1999, Yanga ikiwa tayari imetwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, alitengua matokeo hayo kwa kuiongezea Mtibwa Sugar pointi za mezani, hivyo kuipiku Yanga.

Hatimaye Mtibwa ilipata ubingwa wa mezani.

Mtibwa ilifanikiwa kutetea ubingwa mwaka 2000, kabla ya kupokonywa na Simba msimu uliofuata, ingawa Yanga iliibuka mwaka 2002 na kuutwaa tena ubingwa huo.

Mwaka 2003 Simba iliyokuwa kali zaidi ilifanikiwa kuutwaa tena ubingwa huo na kuutetea mwaka 2004 kabla ya kupokonywa na Yanga 2005 ambao waliutetea 2006.

Mwaka 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya mabadiliko ya kalenda yake, ikitaka Ligi yake iendane na ligi za Ulaya, hivyo ikaamua kuchezesha ligi ndogo ya mpito kumpata bingwa na mwakilishi wa Kombe la Shirikisho, kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Agosti.

Simba iliibuka bingwa wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Yanga kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kufuatia sare ya 1-1.

Lakini msimu uliofuata ikiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifanikiwa kuurejesha ubingwa wake msimu wa 2008 na kutetea msimu uliofuata ikiwa chini ya kocha huyo, ambaye hata hivyo msimu uliopita alitupiwa virago katia mzunguko wa kwanza tu wa ligi na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia mwenzake, Kostadin Bozidar Papic, ambaye alishindwa kubakisha taji Jangwani, baada ya Simba kuchukua kwa kishindo.

Simba ilishinda mechi zote ikiwemo mbili dhidi ya watani wa jadi, Yanga na kutoa sare mbili tu dhidi ya Kagera Sugar Bukoba na African Lyon Dar es Salaam, hivyo kutwaa ubingwa kwa mbwembwe za aina yake na kufanikiwa kuutetea 2010.

Mwaka 2011 taji lilikwenda Jangwani yalipo maskani ya Yanga SC, kabla ya 2012 kuhamia Msimbazi kwa Simba SC.

Mwaka 2013 Yanga walirudisha taji lao na Mei mwaka 2014, Azam FC iliweka historia ya kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa ligi hiyo.

Kuanzia mwaka 2015 Yanga imetwaa taji la VPL kwa misimu mitatu mfululizo, mpaka sasa wakiwa bado ni mabingwa watetezi.

Kwa ujumla Yanga imetwaa jumla ya mataji 27 ya ligi kuu ya Tanzania wakati Simba imetwaa taji hilo mara 18 pekee.

Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa taji la VPL ilikuwa mwaka 2012. Ni tangu wakati huo Simba haikupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa hadi msimu uliomalizika ambapo imepata tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la shirikisho msimu ujao.

Yanga ni mabingwa wa kihistoria Tanzania, rekodi hizi ni za kujivunia kwa kila MwanaYanga.

Uzuri wa timu Yanga ni timu ambayo haina mbwembwe sana nje ya uwanja lakini mafanikio yake yanadhihirisha timu hii kuwa na utamaduni wa kushinda mataji.
ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
57m ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
3h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
6h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
16h ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
21h ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
1d ago
READ MORE β†’
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
1d ago
READ MORE β†’
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
1d ago
READ MORE β†’