Wanasema usiku wa deni haukawii! Kumekucha Jumapili ya Novemba 05 2023 imewadia! Watani wa jadi Yanga na Simba wanachuana leo katika mchezo wa ligi kuu ya NBC utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11 jioni
Ni mechi muhimu kwa Wananchi, mechi ya kusaka alama tatu ili kumuondoa Azam Fc pale juu ya msimamo wa ligi
Kocha Miguel Gamondi na vijana wake wamepata takribani wiki nzima ya kujiandaa na mchezo huo
Ni wazi hautakuwa mchezo mwepesi lakini ushindi ndio matokeo pekee ambayo yatawapa furaha Wananchi
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kukosa ushindi dhidi ya Simba katika michezo miwili iliyopita
Msimu uliopita Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 mchezo wa duru ya pili ligi kuu ya NBC
Watani hao wa jadi wakakutana kwenye fainali ya Ngao ya Jamii jijini Tanga kuelekea msimu huu na mchezo ukamalizika kwa suluhu ya bila ya kufungana na baadae Simba kushinda kwa mikwaju ya penati
Gamondi amesisitiza mchezo wa leo utakuwa mpya, timu yake imeimarika zaidi kuliko ilivyokuwa kwenye Ngao ya Jamii na zaidi wanacheza katika uwanja mzuri ambao utawaruhusu kucheza aina ya soka lao
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na silaha zake zote, nyota wote wako tayari ni suala la Gamondi kuamua nani atumike leo?
Kila la kheri Wananchi, kila la kheri mabingwa wa nchi...!