Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anaamini kikosi chake kina nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Simba siku ya Jumapili kutokana na utayari wanaoonyesha wachezaji wake kuelekea mchezo huo
Gamondi anaendelea kukiandaa kikosi chake Avic Town kuelekea mchezo huo. Amesema licha ya mchezo huo kutarajiwa kuwa mgumu, utaamuliwa na ubora wa wachezaji
Gamondi ana imani na kikosi chake chenye nyota wenye ubora mkubwa ambao wako tayari, wakiahidi kufanya kila kinachowezekana kupata alama tatu
"Ili uwe bora unatakiwa kushinda mechi kubwa na ndogo na huo ni mwendelezo kwani wachezaji wangu wana huo uwezo," Gamondi alinukuliwa na Mwanaspoti
"Simba nawajua nimewaona wakicheza na nimekutana nao pia ila mechi hii itakuwa tofauti, naamini tutafanya vizuri"
"Tunawaheshimu wapinzani wetu kwani wana wachezaji wenye uzoefu ila timu itakayocheza kwa ubora ndio itakayoshinda"
"Mashabiki wetu waje uwanjani kutekeleza wajibu wao wa kuwapa nguvu wachezaji, sisi tuna timu bora na tunaamini tunaweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu kama kila mmoja atafanya majukumu yake ipasavyo"
Yanga inahitaji kushinda mchezo huo ili kujihakikishia kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi na pengine kuwa mwanzo wa safari ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo