Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amesema katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu huu, wamejipanga na wana kila sababu ya kufanya vizuri
Yanga imerejea hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa baada ya kusubiri miaka 25. Aidha msimu uliopita Wananchi waliweka rekodi ya kucheza fainali ya kombe la Shirikisho na kuwa timu pekee kutoka Tanzania kuvaa medali ya CAF baada ya kufikia mafanikio hayo
Mashabiki wa Yanga wana matarajio makubwa kwa timu yao kuona kile walichofanya katika Shirikisho msimu uliopita wanarudia katika ligi ya mabingwa
Arafat amesema mipango na mikakati waliyoweka ni kuona wanafanya vizuri angalau kufika hatua ya robo fainali Yanga ikiwa kundi D pamoja na mabingwa watetezi Al Ahly, CR Beluizdad na Medeama
Wengi wanaamini kundi D ni gumu kwa Yanga kutokana na uwepo wa mabingwa Al Ahly na CR Belouizdad ambayo kwa wastani imekuwa ni kawaida yao kutinga robo fainali
Hata hivyo Arafat amesema Yanga ina kikosi imara ambacho kiko tayari kuchuana na timu yoyote barani Afrika na kupata matokeo mazuri
"Timu yetu ipo tayari kuchuana na yeyote. Tuna wachezaji bora ambao wengi wana uzoefu na mashindano makubwa"
"Tuna wachezaji wengi katika timu ya Taifa Tanzania na katika mataifa mengine ambao wana uwezo wa mashindano makubwa. Tunaamini tunaweza kufanya vizuri na kuvuka hatua ya makundi, " alisema Arafat
Yanga itaanzia kampeni ya hatua ya makundi ugenini kwa mchezo dhidi ya CR Belouizdad ambao utapigwa Novemba 25 huko Algeria