Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amemwagia sifa mshambuliaji kinda Clement Mzize baada ya kufunga bao pekee la ushindi kwenye mchezo wa mkondo wa pili ligi ya mabingwa dhidi ya Al Merrikh ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Al Merrikh hawatamsahau Mzize kwani unaweza kusema ndiye aliyewatupa nje kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na kuipa Yanga tiketi ya kutinga makundi baada ya kufunga mabao mawili kati ya matatu yaliyofungwa na Yanga katika mechi zote mbili
Katika mchezo uliopigwa juzi katika uwanja wa Azam Complex Mzize aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kennedy Musonda, pengine angeweza kuondoka na mabao mawili katika mchezo huo kama bao lake la kwanza lisingekataliwa na mwamuzi baada ya krosi ya Max Nzengeli
"Nampongeza Mzize, umri wake badio mdogo lakini nafurahishwa na maendeleo yake. Ulikuwa ni mkakati kutomuanzisha kwa sababu tulifahamu baada ya kufanya vizuri mchezo wa kwanza, Al Merrikh wangemuwekea mkakati wa kumdhibiti"
"Alipoingia alifanya kile tulichomuelekeza na kutufungia bao muhimu lililotuhakikishia nafasi yetu katika hatua ya makundi," alisema Gamondi
Mzize ni kama anaanza kujihakikishia nafasi katika safu ya ushambuliaji mbele ya Musonda na Hafiz Konkoni ambaye bado anaendelea 'kujitafuta'
Mzize amefunga mabao katika mechi zote za kutafuta tiketi ya kutinga makundi
Alifunga katika mchezo wa pili dhidi ya Asas Fc na pia amefunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Al Merrikh