Mwaka 1998 Mabingwa wa Tanzania, Yanga walikuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kubadili muundo wa mshindano hayo
Wakati huo hatua ya makundi ilikuwa ikishirikisha timu nane tu ambazo zilipangwa katika makundi mawili. Hata hivyo CAF ilibadili tena muundo huo mwaka 2016 ambapo tangu wakati huo timu 16 zinacheza hatua ya makundi badala ya nane ambazo kwa muundo wa sasa ni robo fainali
Jumamosi ijayo, Septemba 30 Yanga ina nafasi nyingine ya kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa katika muundo mpya
Ikiwa mbele kwa mabao 2-0 ushindi waliopata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, Yanga inahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare dhidi ya Al Merrikh ili kutinga makundi
Ni takribani miaka 25 imepita tangu Yanga ilipocheza makundi ya ligi ya mabingwa, hii ndio sababu inayofanya mchezo wa Jumamosi uwe na umuhimu wa kipekee
Wananchi hawana deni kwenye kombe la Shirikisho kwani ni msimu uliopita tu, Yanga ilifanikiwa kufika hatua ya fainali na kukosa ubingwa kikanuni
Tangu mwaka 1998 Yanga ilicheza mara mbili hatua ya makundi ya Shirikisho lakini haikuwahi kuvuka hatua ya makundi kabla ya msimu uliopita ambao iliiheshimisha Tanzania kwa kucheza fainali
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema anafahamu shauku ya mashabiki wa Yanga ni kuona wanafanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa kama ilivyokuwa katika Shirikisho msimu uliopita
Lakini amesisitiza kwa sasa malengo yao ni kutinga makundi ili kumaliza 'ukame' wa miaka 25 na wakifanikiwa kuvuka watakuwa na malengo mengine
"Msimu uliopita ulikuwa wa kihistoria kwetu kwenye kombe la Shirikisho, huu ni msimu mwingine, kwa muda mrefu hatujashiriki hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa, tunataka kwenda makundi"
"Niwaombe Wanachama na Mashabiki wa Yanga tuwe pamoja, tuhakikishe tunajitokeza kwa wingi uwanja wa Azam Complex siku ya Jumamosi ili kuhakikisha tunatinga hatua ya makundi," alisema Hersi