Juzi Yanga ilipunguzwa kasi yake kwenye ligi kuu ikishinda bao 1-0 katika mchezo dhidi ya Namungo Fc uliopigwa uwanja wa Azam Complex
Ulikuwa mchezo wa upande mmoja kwani Yanga ilikuwa ikicheza na Namungo Fc ikizuia na wachezaji 10 (walipaki basi) huku wakitumia mashambulizi ya kushitukiza
Baada ya mchezo huo Mkufunzi wa Yanga Miguel Gamondi alieleza kutofurahishwa na mbinu zilizotumika na wapinzani wake lakini akawasifu wachezaji wake kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi
Gamondi alisema anafurahia ushindani ambao kikosi chake kinaupata lakini akazitaka timu pinzani kuja na akili ya kuwashambuliana na sio kubaki nyuma muda mwingi.
"Ilikuwa vigumu kufanya mambo kama ambavyo tunataka, tumeinadaa timu yetu kushindana lakini unapocheza na timu inayokaa nyuma wakati mwingine ni vigumu kuona ubora"Β
"Tuna timu inayocheza tumejiandaa kukutana na upinzani, lakini ni vizuri tukaona timu pinzani nazo zikitushambulia ili tushindane, haikuwa hivyo, jambo zuri tuliamua kubadilika na kutumia njia za pembeni kutafuta ushindi ambayo ilitusaidia na kufanikiwa," alisema Gamondi
Gamondi amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari kupambana na mpinzani wa aina yeyote na wanafanya kazi kubwa katika kiwanja cha mazoezi ili kuwa bora wakati wote na kupata ushindi katika mechi zenye mazingira magumu kama ilivyokuwa juzi
Gamondi amesema malengo ya Yanga ni kushinda mechi zote pasipo kujali wanafunga mabao mangapi
"Mashabiki wetu hawaji uwanjani wakiwa na matarajio ya kushinda mabao matano kwa kila mchezo, ni lazima tuwe wakweli, wao wanakuja uwanjani wakiwa na matarajio ya kuona timu yao inashinda na hiki ndicho tutaendelea kukipigania"