Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi na benchi la lake la ufundi wanafanya kazi kubwa katika kiwanja cha mazoezi Avic Town kukiandaa kikosi kwa ajili ya kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali msimu huu
Katika mechi chache ambazo Yanga imecheza, tofauti imeonekana, timu inacheza kwa kasi huku wachezaji wakionyesha kuwa na njaa na kiu ya mafanikio
Mpaka sasa, mashabiki wa Yanga wameridhika na kile walichokishuhudia katika mechi nne zilizopita, mbili za ligi kuu na mbili za Ligi ya mabingwa lakini furaha yao itakuwa kubwa zaidi kama wataishuhudia timu yao ikipata ushindi dhidi ya Al Merrikh na kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Ukweli ni kwamba kizazi cha mashabiki wengi vijana wa Yanga hawajaishuhudia timu yao ikicheza makundi ya ligi ya mabingwa, mara ya mwisho Yanga ikicheza makundi mwaka 1998 wakati huo hatua ya makundi ikishirikisha timu nane tu (sasa ni robo fainali)
Gamondi anafahamu kiu kubwa ya Wananchi msimu huu na ndio maana kuna umakini mkubwa sana katika kiwanja cha mazoezi
Pamoja na kucheza fainali ya kombe la Shirikisho msimu uliopita, Wananchi wanafahamu timu yao iliondolewa katika hatua kama hii tena dhidi ya timu nyingine kutoka Sudan (Al Hilal) hivyo mechi dhidi ya Al Merrikh ni kama mechi ya kisasi
Gamondi amesema yeye na benchi lake la ufundi wanafahamu kiu kubwa ya uongozi, wanachama na mashabiki wa Yanga na wamejipanga kufanikisha malengo
"Tunaendelea na maandalizi ya mwisho ya michezo hii ya hatua ya mtoano, nafahamu msimu uliopita tuliondolewa katika hatua kama hii na timu kutoka Sudan, najua kuna zaidi ya miaka 20 timu haijacheza hatua ya makundi, hivyo tunafahamu ugumu na umuhimu wa michezo hii," alisema Gamondi
Yanga inatarajiwa kuondoka Tanzania siku ya Alhamisi kuelekea Rwanda kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza ambao utapigwa Septemba 16 katika uwanja wa Pele, Kigali