Wakati baadhi ya wachezaji wakiondoka kwenda kutimiza majukumu ya timu za Taifa, kikosi cha Yanga jana kilirejea mazoezini kuanza maandalizi ya mchezo wa kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya El Merrikh
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kati ya Septemba 15-17 Yanga ikianzia ugenini na kumalizia mchezo wa pili nyumbani
Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema watakuwa na program maalum ya mazoezi kwa siku mbili kabla ya wachezaji kupewa tena mapumziko mwishoni mwa wiki
Harrison amesema kikosi kitaingia kambini Jumatatu kukamilisha maandalizi ya mchezo huo ambao wamedhamiria kupata matokeo mazuri na kutinga hatua ya makundi
"Baada ya ushindi mnono dhidi ya JKT Tanzania, wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja. Jana timu ilirejea mazoezini kwa wachezaji ambao hawana majukumu ya timu za Taifa"
"Tutafanya mazoezi kwa siku mbili kisha wachezaji watapewa mapumziko siku ya Jumamosi na Jumapili na watarejea tena Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea mchezo husika"
"Kwa kuwa tutakuwa na muda mrefu, tunatarajia kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuwakabili El Merrikh katika mchezo ambao tunahitaji ushindi ili tuweze kutinga hatua ya makundi," alisema Walter
Aidha Walter amesema winga Skudu Makudubela amepona majeraha na tayari ameungana na wenzake katika mazoezi ya timu