Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema kuwa wachezaji wanashauku kubwa na mchezo wa hatua ya awali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Asas Fc ya Djibout
Mchezo huo utapigwa Jumapili, August 20 katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam
Kamwe amesema siku ya Jumapili wanakwenda kutuma salamu kwa timu zote zinazoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu pamoja na ligi kuu ya NBC
"Jumapili tuna jambo letu pale uwanja wa Azam Complex, tunakwenda kutuma salamu kwa timu zinazoshiriki ligi ya mabingwa msimu huu. Kile ambacho tunakwenda kukifanya pia itakuwa salamu kwa timu zinazoshiriki ligi kuu wafahamu zamu yao inafuata"
"Baada ya kile kilichotokea kwenye Ngao ya Jamii, wachezaji walirejea mazoezini wakiwa na nguvu kubwa. Wanaamini bado hawajawaonyesha mashabiki kile walichowaandalia msimu huu. Ndio maana wameisubiri kwa hamu kubwa mechi ya Jumapili"
"Tumezungumza sana kuhusu ubora wa kikosi tulichonacho msimu huu, sasa hatutazungumza tena, watu wataona vitendo tu, na kazi hiyo tunaianza siku ya Jumapili," alitamba Kamwe
Baada ya kurejea kutoka Tanga, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi aliwapeleka wachezaji wake moja kwa moja kambini Avic Town kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mchezo dhidi ya Asas Fc
Jambo la uhakika ni kuwa siku ya Jumapili, Wananchi watarajie kuona sura tofauti ya Yanga hasa inapokuwa kwenye lango la wapinzani