Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu huu, wanahitaji kurudia mafanikio waliyopata kwenye michuano ya kombe la Shirikisho msimu uliopita
Jumapili August 20 Yanga watakuwa wageni wa Asas Fc katika mchezo wa hatua ya awali ambao utapigwa uwanja wa Azam Complex
Kutokana na nchi ya Djibout kutokuwa na uwanja unaokidhi viwango vya CAF, Shirikisho hilo limeagiza mechi zote mbili zipigwe nchini Tanzania
Kamwe amesema mchezo wa siku ya Jumapili ambao Yanga watakuwa ugenini, wanahitaji kutuma ujumbe kwa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo msimu huu
"Kwa miaka mingi hatujawa na rekodi nzuri katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, msimu huu tumedhamiria kuyaleta mafanikio tuliyopata kwenye kombe la Shirikisho msimu uliopita"
"Siku ya Jumapili tunakwenda kuzitumia ujumbe timu zinazoshiriki ligi ya mabingwa msimu huu, kuwa Wananchi tuko tayari kwa michuano hiyo," alitamba Kamwe
Mchezo wa kwanza utapigwa August 20 wakati mchezo wa marudiano utapigwa August 28 hapohapo kwenye uwanja wa Azam Complex
Kama Yanga itavuka hatua ya awali, mechi za raundi ya kwanza watacheza na mshindi wa mchezo kati ya Otoho (Congo) dhidi ya El Marreikh ya Sudan