Wananchi Yanga wako mkoani Tanga ambapo leo majira ya saa 1 usiku watashuka uwanja wa Mkwakwani kumenyana na Azam Fc katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali Ngao ya Jamii
Kwa mara ya kwanza, Ngao ya Jamii inahusisha timu nne, mechi mbili za nusu fainali zitapigwa. Singida FG ikitarajiwa kumenyana na Simba hapo kesho katika mchezo wa pili wa nusu fainali
Wakiwa ni mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii kwa misimu miwili mfululizo, Yanga imepania kuirudisha Ngao hiyo katika makabati yake pale Jangwani kwa msimu wa tatu mfululizo
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi mbele ya Azam Fc ambayo inaendelea kusaka nafasi kwenye ufalme wa soka la Tanzania
Azam Fc wamekuwa na maandalizi mazuri ikiwa ni pamoja na kuweka kambi huko Tunisia, pia wamefanya usajili mzuri. Miongoni mwa wachezaji waliowasajili ni Feisal Salum na Yannick Bangala ambao walikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu uliopita
Utakuwa mchezo wa kwanza wa mashindano kwa kocha Miguel Gamondi ambaye nae kikosi chake kimeimarishwa zaidi katika dirisha la usajili
Pengine mchezo wa leo utawapa mashabiki wa Yanga taswira halisi ya nini wakitarajie kutoka kwa timu yao msimu huu
Katika mechi tano zilizopita zilizokutanisha Yanga na Azam Fc, takwimu zimekuwa bora upande wa Wananchi, Yanga imeshinda mechi nne na sare moja
Kwa Azam Fc, mechi dhidi ya Yanga wanaichukulia kwa uzito mkubwa zaidi pengine kuliko mchezo wowote
Upinzani baina ya timu hizi unaongezeka mwaka hadi mwaka. Hata hivyo wanakutana na Yanga ambayo iko imara na ina malengo makubwa zaidi kwenye soka la Afrika