Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amewaomba Wanachama na mashabiki waendelee kuwa na imani na uongozi wake kwani wamejipanga kuendeleza mafanikio waliyopata msimu uliopita
Leo Hersi ametimiza mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Yanga Julai 10 2022
Akizungumza katika hafla ya Yanga kukabidhiwa Tsh Milioni 405 na Wadhamini SportPesa baada ya kutwaa mataji matatu msimu uliopita, Hersi amesema mafanikio yaliyopatikana yalitokana na umoja na ushirikiano wa timu pamoja na wadhamini wao
"Leo ninapozungumza hapa nimetimiza mwaka mmoja tangu Wanachama mliponiamini na kunichagua kuwa Rais wa klabu hii. Naomba mnipe imani hiyo katika miaka mingine mitatu iliyobaki ili tuendeleze yale mazuri tuliyofanya"
"Niwahakikishie tumejipanga, Mashabiki wetu wasitishwe na kelele huko mitandao kwani sisi tulishatoka huko. Tuna timu imara ambayo kwa maboresho tuliyofanya, msimu ujao tutakutana tena hapa kupongezana kwa mafanikio mengine," alisema Hersi
Hersi ameishukuru kampuni ya SportPesa kwa kutimiza wajibu wake wa kimkataba baada ya kutoa bonas ya Tsh Milioni 405
"Sisi na SportPesa tuna makubaliano ya aina mbili. Kuna malipo ambayo tunapata kila mwezi lakini kuna malipo ambayo yanatokana na mafanikio ya timu, bonas hii inatokana na mafanikio tuliyopata msimu uliopita kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu, Ngao ya Jamii na kombe la FA pamoja na kufika fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika"