Baada ya kuwasili Algeria hapo jana, kikosi cha Yanga leo kitakamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa mkondo wa pili fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger
Ni mchezo wa kuamua hatma ya ubingwa wa CAF CC katika uwanja wa July 05 1962, muda wa mchezo utakuwa saa 4 usiku kwa saa za Tanzania ambapo huko Algiers itakuwa saa 2 usiku
Yanga itahitaji kufunga angalau mabao mawili bila majibu ili kutwaa taji hilo na kuandika rekodi ya kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki
Yanga itaingia uwanjani hapo kesho ikiwa na sapoti kubwa ya mashabiki zaidi ya 200 waliosafiri na timu pamoja na Watanzania wanaoishi Algeria
Ni wazi itakuwa mechi ya kufa au kupona kwa Yanga, Wananchi hawatakuwa na cha kupoteza zaidi ya kusaka ushindi
Hii ni mechi ambayo wachezaji wanaitaka kwelikweli kwa sababu wanajua thamani yake
Ni heshima kwa wachezaji wa Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo lakini itakuwa heshima kubwa zaidi kama watafanikiwa kutwaa ubingwa
Majina yao yataandikwa kwa wino wa dhahabu katika vitabu vya kumbukumbu vya klabu ya Yanga
Vizazi na vizazi vitahadithiwa kile walichofanya Juni 03 2023 nchini Algeria kwa kutwaa taji la CAF CC wakiwa ardhi ya ugenini