Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi wanafahamu kikosi chao kinahitaji kushinda kwa mabao mawili nchini Algeria ili kuwa na nafasi ya kutwaa taji la Cofederation barani Afrika
Yanga inakamilisha maandalizi yake hapahapa Tanzania kabla ya kusafiri kwenda Algeria tayari kwa mchezo wa pili wa fainali dhidi ya USM Alger ambao utapigwa Jumamosi, Juni 03, saa 4 usiku
Nabi amesisitiza kuwa inawezekana kushinda Algeria na muhimu ni kwa wachezaji wake kupambana kwa dakika zote 90
Takwimu za Yanga kwenye mechi za ugenini katika mashindano ya CAF msimu huu zinawapa Wananchi jeuri na kuamini INAWEZEKANA
Tangu hatua za awali Ligi ya Mabingwa na baadae makundi kombe la Shirikisho, robo fainali na nusu fainali, Yanga imepoteza mechi mbili tu
Ilifungwa na Al Hilal 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ligi ya mabingwa na pia kufungwa na US Monastir 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Shirikisho
Mechi za ugenini ambazo Yanga ilishinda ni dhidi ya Club Africain (1-0), TP Mazembe (1-0), Rivers United (2-0), Marumo Gallants (2-1) huku ikilazimishwa sare katika mchezo dhidi ya Real Bamako(1-1)
Kwenye Shirikisho Yanga imepoteza mechi moja tu ugenini na kutoka sare mechi moja huku ikishinda mechi nne
Katika mashindano haya, USM Alger wameshinda mechi zote walizocheza katika uwanja wao wa nyumbani lakini pia ilikuwa hivyo kwa Rivers United na Marumo Gallants
Yanga imeweza kuvunja rekodi za timu hizo na hakuna shaka inaweza kuvunja rekodi ya USM Alger na kutwaa taji la CAF CC mbele ya mashabiki wao