Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema wachezaji wake hawana hofu yoyote kuwakabili Marumo Gallants katika uwanja uliojaa mashabiki baada ya timu hiyo kuondoa viingilio kwenye mchezo wa mkondo wa pili nusu fainali ya kombe la Shirikisho ambao utapigwa kesho Jumatano huko Afrika Kusini
Akizungumza katika Mkutano wa mechi, Nabi alisema wanafurahi, wachezaji wake wana uzoefu kucheza kwenye uwanja wenye mashabiki wengi kuliko uwanja mtupu
"Ni jambo zuri Marumo wamepanga mechi isiwe na kiingilio. Sisi kama Yanga tunapenda kucheza mbele ya mashabiki wengi kuliko uwanja kukosa mashabiki. Nina wachezaji wenye uzoefu wa kutosha wa kucheza mechi za namna hii," alisema Nabi
Aidha Nabi amebainisha kuwa wanakwenda kuikabili Marumo Galllants pasipo kujali matokeo waliyopata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kwani anatambua huo ni mchezo tofauti ambao unahitaji mipango tofauti pia
"Tumesahau kuhusu faida ya ushindi wa 2-0 tulioupata kwenye uwanja wa nyumbani. Huu ni mchezo mwingine na tuko na mpango mwingine wa dakika 90 za hapa"
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, mshambuliaji Kennedy Musonda amesema wako tayari kwa mchezo mkubwa na lengo lao ni kurudi na ushindi Tanzania
"Maandalizi ni mazuri sana kwa upande wetu wachezaji na tunajua tumekuja kwenye mchezo mkubwa. Tuko tayari kupambana na kurudi nyumbani tukiwa washindi"