Jana Yanga iliendeleza umwamba kwenye michuano ya Shirikisho ya CAF ikiichapa Marumo Gallants katika mchezo wa mkondo wa kwanza nusu fainali uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Mabao ya Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison yalitosha kuihakikishia Yanga ushindi muhimu ambao unawaweka mbele kuelekea mchezo wa mkondo wa pili ambao utapigwa wiki ijayo huko Afrika Kusini
Katika mchezo huo Yanga itahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare kuweza kutinga fainali
Katika mchezo dhidi ya Marumo jana, Yanga iliweka rekodi nyingine ya kibabe
Ni hivi Wananchi wamecheza mechi sita mfululizo kwenye mashindano hayo pasipo kuruhusu bao
Mara ya mwisho Yanga kuruhusu bao katika mashindano hayo, ilikuwa kwenye hatua ya makundi walipolazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako nchini Mali
Mechi ya marudiano dhidi ya Real Bamako jijini Dar es salaam, Yanga ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0, wakaja US Monastir nao wakachapwa mabao 2-0
Zamu ya TP Mazembe ikafuata wakachapwa bao 1-0 kwao, Rivers United nae akapigwa 2-0 kwao kabla ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa pili wa robo fanali uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ni mchezo wa sita mfululizo Yanga inaondoka na cleansheet
Aidha Yanga imekuwa klabu ya kwanza kuizuia Marumo Gallants kufunga bao kwani kabla ya jana, walifunga bao katika kila mchezo katika michuano hiyo