Baada ya mapumziko ya siku moja, kikosi cha Yanga kimerejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Rivers United. Mchezo huo utapigwa Jumapili, April 30 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema wachezaji wote wamerejea mazoezini kukamilisha maandalizi ya mchezo dhidi ya Rivers United
"Baada ya kurejea kutoka Nigeria wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja, kikosi kimerejea mazoezini leo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa pili dhidi ya Rivers United ambao utachezwa Jumapili pale uwanja wa Benjamin Mkapa"
"Tunashukuru wachezaji wote wako sawa, hatukupata mchezaji majeruhi kwenye mchezo wetu wa kwanza," alisema Kamwe
Kamwe amesema wachezaji wamerejea mazoezini wakiwa na morali ya hali ya juu dhamira yao ikiwa kushinda mechi ya Jumapili ili watinge nusu fainali
"Baada ya ushindi kule Nigeria sisi viongozi tulishangilia sana lakini hali ilikuwa tofauti kwa wachezaji. Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto alisema furaha yao ni baada ya mchezo wa pili dhidi ya Rivers United Jumapili"