Yanga tayari iko katika Mji wa Uyo ambako mchezo dhidi ya Rivers United utapigwa siku ya Jumapili
Ni mchezo muhimu wa mkondo wa kwanza robo fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Yanga imekwenda Nigeria ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi zote mbili za hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Rivers United mwaka 2021
Hivyo Wananchi wametua Nigeria wakiwa na dhamira moja tu, kusaka ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali kwani dakika 90 za pili zitahitimishwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, April 30
Yanga imeonyesha ubora mkubwa katika hatua ya makundi, ikiibuka kinara wa kundi D baada ya kufikisha alama 13
Matumaini ya Wananchi yanabebwa na ubora huo kwani kama Yanga itacheza kama ilivyocheza mechi zake tano zilizofuata baada ya kupoteza dhidi ya US Monastir, wana nafasi nzuri ya kuwaondoa Rivers United
Rivers United walimaliza nafasi ya pili kundi B wakiwa na alama 10 nyuma ya ASEC Mimosas, nao walionyesha ubora katika mechi zao hasa walizocheza nyumbani
Timu zote zimebadilika kwani kama ilivyo kwa Yanga, hata Rivers United kikosi walichonacho sasa sio kile walichokuwa nacho mwaka 2021
Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wanafahamu ubora wa Rivers United lakini pia Yanga nayo ina ubora wake hivyo wako tayari kuwakabili kwenye mchezo utakaopigwa Jumapili, saa 10 jioni katika uwanja wa Godswill Akpabio International