Achana na Fiston Mayele ambaye Simba wanaamini ndiye mchezaji wanayepaswa kumuhofia zaidi kwenye kikosi cha Yanga kuelekea mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili, April 16 2023
Yawezekane wanamuhofia zaidi Mayele kwa sababu ameshawatungua mara tatu lakini wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda, Bernard Morrison hata Jesus Moloko wanaweza kuwa hatari zaidi katika mchezo huo
Yanga ina wachezaji wengi wa 'mechi kubwa' ambao Kocha Nasreddine Nabi anaweza kuwatumia kuiadhibu Simba kama alivyofanya katika mechi zilizopita
Katika mechi nane alizokutana na Simba, Nabi alipoteza mechi moja tu ya nusu fainali kombe la FA kule mkoani Kigoma katika mchezo ambao Yanga ilicheza dakika 45 za kipindi cha pili ikiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya Mukoko Tonombe kutolewa nje kwa kadi nyekundu
Musonda aliyetua Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo, ametengeneza pacha ya aina yake na Mayele katika mechi za kombe la Shirikisho akiwa amefunga mabao mawili na kutoa assist tatu
Musonda hakuonekana kuwa na madhara sana kwenye 'mechi za kawaida' lakini amejipambanua kuwa mchezaji wa mechi kubwa
Aliwatungua TP Mazembe na US Monastir huku akitoa pasi za mabao katika mechi dhidi ya TP Mazembe, Real Bamako na US Monastir
Aziz Ki yeye anarekodi ya aina yake hasa anapokutana na Simba. Aliwatungua mabao mawili wakati akiitumikia Asec Mimosas katika michuano ya kombe la Shirikisho msimu uliopita
Msimu huu Aziz Ki alitengeneza bao moja la Mayele katika mchezo wa Ngao ya Jamii na ndie aliyefunga bao la kuisazishia Yanga katika mchezo wa duru la kwanza
Aziz Ki anakwenda kuikabili Simba wakati morali yake ikiwa juu akitoka kufunga hat-trik katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar
Morrison amerejea hivi karibuni baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa takribani miezi minne. Yawezekana Nabi asimuanzishe lakini atakapoingia atawaweka waajiri wake hao wa zamani katika nyakati ngumu
Moloko amekuwa katika kiwango bora sana msimu huu. Ana bao moja na assist mbili kwenye kombe la Shirikisho. Amejipambanua kuwa mchezaji hatari miongoni mwa mawinga wa Yanga
Yanga pia inajivunia ubora wa safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa haifungiki kirahisi. Djigui Diarra, Djuma Shabani, Bakari Nondo Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Yannick Bangala, Joyce Lomalisa, Kibwana Shomari, Khalid Aucho, Sure Boy, Mudathir, Mauya na wengine wameifanya Yanga kuwa timu ngumu kufungika kirahisi msimu huu
Yanga imeshinda mechi 13 mfululizo katika ligi kuu ya NBC, lakini pia imefunga bao katika kila mchezo wa ligi msimu huu!