Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema wanajiamini kuelekea mechi za robo fainali kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya Rivers United ndio maana walifurahia baada ya droo iliyofanyika huko Misri
Baadhi ya wachambuzi wamekosoa kitendo cha mashabiki na baadhi ya viongozi kushangilia baada ya Yanga kupangwa kucheza na Rivers United
"Sisi tunajiamini tuna timu bora, sio Rivers United tu, tungeshangilia hata kama tungepangwa na timu nyingine kwani kwenye mashindano haya tumejipanga kufanya makubwa hatumuhofii yeyote"
"Mechi dhidi ya Rivers United ina umuhimu wa kipekee kwetu kwa sababu hii itakuwa nafasi kwetu kulipa kisasi. Sote tunakumbuka walichotufanyia kwenye michuano ya ligi ya mabingwa miaka miwili iliyopita. Sasa tunasema kisasi ni haki!," alitamba Kamwe
Katika hatua nyingine, kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanja wa Azam Complex, siku ya kesho Jumamosi katika mchezo wa robo fainali kombe la FA dhidi ya Geita Gold
Kamwe amesema wanahitaji kushinda mchezo huo ili kutinga nusu fainali, anaamini hilo litawezekana kutokana na ubora wa timu yao pamoja na nguvu ya mashabiki
"Tunawaomba mje kwa wingi uwanja wa Azam Complex kama mlivyofanya kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Geita Gold. Tunahitaji kushinda mchezo huu ili twende nusu fainali"