Kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' anapaswa kufanya maamuzi kwa mustakabali wa hatma yake katika mpira wa miguu
Tayari amefanya makosa makubwa kwa kuruhusu kukaa miezi mitatu nje ya uwanja pasipo kucheza mpira
Imefanyika kamali ya kumjumuisha kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ambacho jana kilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Uganda
Jana Feisal alikuwa uwanjani kwa takribani dakika 20 huku akitumika kwa takribani dakika 10 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Misri ambao Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Dakika 30 alizocheza katika mechi hizo mbili zinapaswa kumuonyesha nini kitatokea kwake kama ataendelea kuwa 'mkaidi' kwani kukaa kwake nje kunamuathiri yeye mwenyewe na sio Yanga
Wakati yeye kiwango chake kikiendelea kuporomoka, Yanga imeendelea kuwa bora na pengine hata akirejea leo hataweza kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza
Prof Helmy Gueldich atakuwa na kazi ya ziada kuirejesha 'fitness' yake iliyopotea kabla ya Nasreddine Nabi kumfikiria kumtumia kwenye kikosi cha kwanza
Yanga imeshaweka wazi haimlazimishi Feisal kuitumikia lakini akirejea atapokelewa kwa sababu bado ana mkataba utakaofikia tamati May 30 2024
Na kama anahitaji kuondoka ni vyema yeye mwenyewe au klabu inayotaka kumsajili wakaenda mezani kumalizana na Yanga ili awe huru kuondoka
TFF imethibitisha mara mbili kuwa ana mkataba na Yanga, kurejea tena TFF kuomba mkataba uvunjwe ni kuendelea kupoteza muda kwa kuwa haipo sababu ambayo itafanya TFF wauvunje mkataba huo kwani tayari wameshaupitia na kujiridhisha hauna kasoro
TFF wanaweza kumsaidia kwa kumwambia nenda kazungumze na waajiri wako mkubaliane!
Inasikitisha sana kwa mchezaji aliyekuwa amefika kiwango cha juu kabisa katika maisha yake ya soka anakwenda kupotea kwa kuweka mbele maslahi yake zaidi kuliko ya wale waliomtengeza kufika hapo alipo
Feisal au kama wapo watu ambao wako nyuma ya sakata lake lazima wafahamu, ni Yanga iliyomfanya aonekane bora, kuna kazi kubwa ilifanyika kutoka benchi la ufundi la Yanga kumuandaa Feisal
Yanga ina haki ya kimsingi ya kutetea maslahi yake, kama Feisal anaamua kuondoka basi lazima afate utaratibu kwa kuwalipa Yanga gharama ambazo wametumia
Gharama hizo wanazifahamu Yanga wenyewe ndio maana wakamwambia kama unataka kuondoka njoo mezani tuzungumze lakini pia ruksa kurejea kazini huku wakimpa ahadi ya kumboreshea maslahi yake