Kesho Jumanne timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kupepetana na Uganda katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afcon 2023
Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Clifford Mario Ndimbo ametangaza kuwa tiketi zote za Mzunguuko zimenunuliwa hivyo Watanzania wataruhusiwa kuingia bure
Leo Machi 27, 2023, Kamati ya Hamasa ya kuchangia tiketi kwa ajili ya mchezo huo, ikiongozwa na Ndimbo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally pamoja na Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, imekusanya tiketi 9545 kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka na kufikisha idadi ya tiketi 51,545 ikiwa ni pamoja na tiketi 42,000 zilizokusanywa awali zikiwemo za Serikali
"Eneo la mzunguko tayari limeshajaa, kuanzia saa 6:00 mchana milango itakuwa wazi kwahiyo Mtanzania yoyote popote ulipo kuwahi kwako kufika ndio kuingia kwako. Kwenye eneo la mzunguko, kila mtanzania ana nafasi ya kuingia uwanjani kwakuwa tayari zimeshalipiwa"
"Kama tiketi zingekuwa chache tungetangaza utaratibu wa namna ya kupata lakini kwakuwa tayari zimenunuliwa zote basi milango ipo wazi kwa wote," alisema Ndimbo
Mchezo unatarajiwa kupigwa kuanzia saa 2 usiku