Kocha Mkuu wa Yanga Nasrddine Nabi atakuwa akitabasamu huko aliko pale anapoona beki wake Ibrahim Bacca akimwagiwa sifa kemkem kutokana na kiwango alichoonyesha katika mechi mbili zilizopita
Ni mwendelezo wa Nabi kuibua vipaji kutoka katika kikosi chake, kwa hakika huyu ni Profesa wa 'boli'
Dakika 180 zimetosha kumtambulisha Bacca kwenye soka la Tanzania na pengine kufungua rasmi ukurasa wake wa mafanikio
Iliotolewa orodha ya wachezaji 11 wanaoanza mchezo dhidi ya US Monastrir jina la Bacca lilichomoza katika safu ya ulinzi. Wapo waliohoji huyu Nabi vipi?
Ikiwa ni mechi muhimu ya kombe la Shirikisho barani Afrika kwa Yanga kushinda ili kutinga robo fainali, wengi hawakutarajia kumuona Bacca katika mchezo huo uliokuwa na presha kubwa
Lakini historia ilibadilika baada ya dakika 90, Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 Bacca akin'gara kwenye safu ya ulinzi
Baada ya mchezo huo, jina la Bacca likaonekana kwenye orodha ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ambao wataikabili Uganda kwenye mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2023
Juzi mechi ya kwanza dhidi ya Uganda ikapigwa Misri, kwa mara ya pili jina la Bacca likaonekana kwenye safu ya ulinzi akianza sambamba na pacha wake Bakari Nondo Mwamnyeto huku Dickson Job akihamishiwa upande wa kulia
Zikawa dakika nyingine 90 bora kwa Bacca, kila alichofanya kwenye mchezo huo kilikuwa sahihi! Bacca ni mchezaji aliyepokea sifa nyingi baada ya dakika 90 za mchezo ule
Amekuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha Nabi kabla lakini hakuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa kama itakavyokuwa sasa