Simon Msuva ameifungia Tanzania goli pekee la ushindi katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon 2023 dhidi ya Uganda
Krosi murua kutoka kwa Dickson Job aliyetumika kama mlinzi wa kulia ilitua mguuni kwa Msuva naye bila ajizi kuweka mpira kambani na kuihakikishia Stars ushindi wa bao 1-0
Kiwango bora kwa wachezaji wote wa Stars lakini kwa hakika safu ya ulinzi chini ya Bakari Nondo Mwamnyeto na Ibrahim Bacca walicheza vizuri wakisaidiana na walinzi wa pembeni Dickson Job na Novatus Dismas huku mbele yao wakikaa viungo watatu Mudathir Yahya, Mzamiru Yassin na Himid Mao
Ni mechi yake ya kwanza kwa Bacca kuitumikia timu ya Taifa lakini bila shaka leo amejihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kocha Adel Amrouche
Stars inarejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda ambao utapigwa Jumanne, March 28
Alama nne kwa Tanzania katika nafasi ya pili kundi F. Ushindi mwingine siku ya Jumanne itaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa michuano ya Afcon 2023 itakayofanyika Ivory Coast

