Majira ya saa 1 usiku Wananchi watashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuumana na US Monastir katika mchezo wa kombe la Shirikisho ambao huenda baada ya dakika 90 Yanga ikaweka mkononi tiketi ya kutinga robo fainali
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi jana alibainisha kuwa pamoja na kuwa wanahitaji kushinda mchezo huo, watacheza kwa tahadhari na umakini kuhakikisha hawawapi nafasi US Monastir kufunga bao mapema
Katika mechi nne walizocheza katika kundi D, Monastir walifunga bao ndani ya dakika 15 za kwanza katika mechi dhidi ya Yanga na TP Mazembe ambao waliwafunga mara mbili
Monastir wamefunga bao katika kila mchezo huku wakiruhusu bao moja tu kutikisa nyavu zao
Huanza mechi kwa kasi kubwa na pale wanapofanikiwa kufunga basi hurudi nyuma kulinda ushindi na kutumia mashambulizi ya kushitukiza
Lakini pia silaha kuu ya timu hii ni mipira ya kutenga, iwe kona au adhabu, wanafunga mabao mengi ya vichwa kupitia mipira hiyo
Yanga inakumbuka kilichotokea kule Tunisia kwenye mchezo wa kwanza, Monastir walicheza mechi ile kwa takribani dakika 20 tu
Ndani ya muda huo walifanikiwa kufunga mabao mawili yote yakitokana na mipira ya kichwa
Nabi amesema wamefanya kazi kubwa kwenye viwanja vya mazoezi, ana imani leo wachezaji wake watakuwa makini katika kukabiliana na aina hiyo ya mipira
Yanga imeweka rekodi ya aina yake katika mechi walizocheza dimba la Mkapa. Ndani ya dakika 10 wamefunga mabao katika mechi dhidi ya TP Mazembe na Real Bamako
Kama Yanga itafunga bao la mapema leo ni wazi watawavuruga Monastir ambao wanasaka angalau alama moja ili wajihakikishie kumaliza vinara wa kundi
Itakuwa mechi ngumu lakini kama mashabiki watajitokeza kwa wingi dimba la Mkapa na kushangilia kwa nguvu, huenda Monastir wakakutana na dakika 90 ngumu zaidi