Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema maandalizi kuelekea mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya US Monastir yanaendelea vizuri
Kamwe amesema mpaka sasa hakuna majeruhi wapya, wachezaji wakiendelea vyema na mazoezi kuelekea mchezo huo
"Nafurahi tunakwenda kucheza na US Monastir tukiwa katika wakati mzuri. Hatuna majeruhi wapya, Morrison alishaanza mazoezi binafsi na pengine leo ataungana na wenzake kwenye mazoezi ya timu"
"Mlinda lango Aboutwalib Mshery ameanza kutembea bila magongo ikiwa ni hatua ya kwanza kwake kabla ya kuanza mazoezi ya utimamu wa mwili"
"Nimezungumza na Meneja wa timu, Walter Harrison amesema wachezaji wako tayari na wanautaka mchezo kwelikweli," alisema Kamwe
Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kuendelea kununua tiketi kwa wingi ili kuhakikisha wanaujaza uwanja wa Benjamin Mkapa kwani tayari wapinzani wao US Monastir wameingia hofu
"Monastir walitua Alfajiri ya leo, wakati kocha wao anafanya mahojiano na wanahabari aliuliza kama uwanja wa Benjamin Mkapa utajaa. Baada ya Wanahabari kumhakikishia kuwa dimba litajaa, akasema kwake itakuwa mara ya kwanza na hata kwa wachezaji wake kushiriki mechi dimba likiwa 'full house' "
"Hivyo mashabiki wetu waone ni kwa kiasi gani wapinzani wetu wanahofia wingi wao katika mchezo huo, hivyo tununue tiketi tuhakikishe uwanja umejaa"