Klabu ya Yanga imeshusha bei ya baadhi ya bidhaa zake kuelekea mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Real Bamako ambao utapigwa baadae leo katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema wameshusha bei ya bidhaa za klabu zinazopatikana kwenye duka la Yanga lililopo Jangwani jijini Dar es salaam
Kamwe amesema ofa hiyo maalum kwa ajili ya kuwawezesha mashabiki kununua jezi, skaf, bendera, mabegi, kofia na bidhaa nyingine ili kuhakikisha uwanja wa Mkapa jioni ya leo unapendeza kwa rangi za njano, kijani na nyeusi
"Mwananchi fika Makao Makuu ya klabu, Jangwani ujipatie jezi, skaf, bendera na bidhaa nyingine kibao kwa bei karibu na bure. Siku ya leo tunataka kuupamba uwanja kwa rangi za njano na kijani. Hakikisha unakwenda uwanjani ukiwa umependeza na uzi wa Yanga" alisema Kamwe
Aidha, klabu ya Yanga imeendelea kugawa tiketi bure kwa Wanawake ikiwa ni zawadi maalum kwao katika siku hii ya Wanawake
Kamwe amesema Wanawake watakaowahi kufika uwanjani watapatiwa tiketi bure
Shamrashamra kuelekea mchezo dhidi ya Real Bamako zitaanza saa 10 jioni kwa burudani kibao zilizoandaliwa