Wakati kikosi cha Real Bamako kutoka Mali kikiwasili nchini alfajiri ya kuamkia jana, Klabu ya Yanga imeweka mkakati wa kuhakikisha inaibuka na ushindi mnono katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Mkurugenzi wa Mashindano wa Klabu hiyo, Saad Kawemba, amesema maandalizi yote kuelekea mchezo dhidi ya Real Bamako yamekamilika na sasa wanachosubiri Jumatano ambapo mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 1:00 usiku, ikiwa ni ya raundi ya nne ya Kundi D
"Maandalizi yote ya mchezo huo yameshakamilika, mchezo ni Jumatano, wageni wetu wameshawasili. March 08 tunahitaji kutoa furaha si kwa wanachama na mashabiki wa Yanga tu, bali kwa Watanzania wote. Tunataka tufanye zaidi ya vile tulivyofanya kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe, tunachoomba ni watu kujitokeza kwa wingi," alisema Kawemba
Kimahesabu Yanga inaweza kujihakikishia tiketi ya kutinga robo fainali ya kombe la Shirikisho kama itashinda mechi dhidi ya Real Bamako na mchezo utakaofuata dhidi ya US Monastir ambayo yote itapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga, inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D kwa pointi nne, na iwapo itashinda itafikisha pointi saba sawa na vinara US Monastir ya Tunisia ambao siku hiyo watakuwa nyumbani huko Tunisia kuikabili TP Mazembe inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi zake tatu
Kama TP Mazembe itapoteza mchezo huko Tunisia basi kazi ya Yanga kwenda robo fainali itakuwa rahisi kwani watahitaji kushinda mechi hizi mbili zinazopigwa mfululizo nyumbani