Nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amesema wanatarajia mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Real Bamako ambao utapiga kesho Jumapili huko Mali utakuwa mgumu
Hata hivyo Mwamnyeto amesema wamefanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri huku akiwataka mashabiki wa Yanga nchini Tanzania wawaombee dua
"Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu tuko ugenini na wenyeji wetu watataka kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kusaka ushindi. Lakini sisi tumejipanga na tutapambana ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri"
"Nawaambia mashabiki wetu Tanzania sisi tuko tayari kwa mchezo jambo muhimu kwao ni kuendelea kutuombea dua ili tuweze kupata matokeo mazuri," alisema Mwamnyeto
Akizungumzia mapokezi ya timu katika Mji wa Bamako, Mwamnyeto amesema uwepo wa wachezaji Djigui Diarra na Mamadou Doumbia umewafanyia mambo mengi kuwa rahisi kwani wamepata sapoti kubwa
"Diarra na Doumbia wametoka hapa, watu wa huku wamefurahi sana kuwaona jambo ambalo limetupa imani kwani mashabiki wanatuunga mkono kupitia wao. Naamini watatusaidia sana hata siku ya mchezo"
Klabu ya Stade Malien ambao ni wapinzani wakuu wa Real Bamako ilitoa uwanja wa mazoezi kwa Yanga na hivyo Wananchi kukwepa mtego wa wenyeji wao ambao waliwapa uwanja wa nyasi bandia ambao haukuwa katika ubora
Ikumbukwe Diarra na Doumbia wamekulia kwenye academy ya Stade Malien na baadae kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio
Katika Mji wa Bamako Diarra anafahamika zaidi kama 'Kamanda'