Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amesema kupoteza mchezo dhidi ya US Monastir ni sehemu ya matokeo lakini hawapaswi kuondoka katika malengo kwani bado wana alama 15 za kugombania
Arafat amesema matokeo hayo yamewafanya wajipange zaidi kuelekea mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa Jumapili ijayo, Februari 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Arafat amewataka mashabiki wa Yanga kutokuwa wanyonge na badala yake wanunue tiketi kwa wingi kuelekea mchezo dhidi ya Mazembe Jumapili
"Kupoteza dhidi ya US Monastir kwa mabao 2-0 hakujatuondolea malengo yetu ya kutinga Hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika"
"Matokeo haya tunayapokea kama njia ya kujipanga kwa uimara zaidi kabla ya kukutana na TP Mazembe Jumapili Februari 19 nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa"
"Uongozi wetu upo makini kuzipa uzito mechi zote 6 za hatua ya makundi na kikosi chetu kitarudi imara tutakapokutana dhidi ya Mazembe. Uzuri wa hizi mechi sio kama zile za mtoano, hapa unatakiwa kujipanga utachukuwaje pointi zako kwa ujumla wake ndani ya mechi sita utakazocheza ambazo tatu zipo nyumbani na tatu ugenini"
"Mashabiki wetu wasijiondoe kwenye malengo yetu, uongozi wao na timu yao tuko makini,watambue kwamba kuna timu iliwahi kufungwa mechi tatu kati ya sita ikaruhusu zaidi ya mabao kumi lakini bado wakafuzu hatua inayofuata"
"Makocha wetu wanajua wapi tumekosea wachezaji wanajua wapi walikosea wanarudi kambini kujiandaa kwa uzito wake dhidi ya Mazembe ninachowaomba mashabiki wetu wasihadaike na kelele zozote wajipange kuja kuipa nguvu timu yao Jumapili Uwanja wa Mkapa," alisema Arafat