February 12 2023 Yanga itacheza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya US Monastir
Mchezo huo utapigwa Tunisia katika uwanja Hammedi Agrebi Olympic, uwanja uleule ambao Yanga walicheza na Club Africain wakaibuka na ushindi wa bao 1-0
Mechi ya pili itapigwa February 18 dhidi ya TP Mazembe katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema katika michuano ya mwaka huu wamedhamiria kufanya vizuri mkakati ukiwa kushinda mechi zote tatu za nyumbani na kusaka angalau alama tatu ugenini ili kutinga robo fainali
Baada ya uzinduzi wa jezi maalum kwa ajili ya michuano hiyo, Kamwe amesema wataanza mapema kuuza tiketi kuelekea mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya TP Mazembe
"Katika hatua ya makundi kila timu imejipanga kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kushinda mechi zote tatu na kutafuta angalau alama tatu katika michezo ya ugenini. Tunawaomba wapenzi na wanachama wetu watuunge mkono kuelekea mchezo dhidi ya Monastir lakini mchezo dhidi ya TP Mazembe utakuwa wa kihistoria na umuhimu wa kipekee"
"Ni mchezo wetu wa kwanza hatua ya makundi kombe la Shirikisho baada ya muda kidogo hivyo tunahitaji hamasa ya mashabiki wetu ili kuhakikisha tunashinda. Tayari tumeandaa utaratibu wa upatikanaji wa tiketi na tutaanza kuziuza mapema"
"Tunataka kuona mashabiki 60,000 wanajitokeza uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao," alisema Kamwe
Mwitikio wa mashabiki umekuwa mkubwa katika kununua jezi maalum kwa ajili ya michuano ya kombe la Shirikisho